19 Februari 2022 - 11:06
Watu 17 wafariki dunia katika mlipuko wa lori la mafuta nchini Nigeria

Kwa akali watu 17 wamepoteza maisha yao katika tukio la mlipuko wa lori la mafuta katika jimbo la Ogun, kusini magharibi mwa Nigeria.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Duru za Nigeria zinaripoti kuwa, mlipuko huo mkubwa ulitokea baada ya lori hilo la mafuta kugongana na gari jingine katika jimbo la Ogun lililoko kusini magharibi mwa Nigeria na kusababisha maafa makubwa.

Timu za uokozi na utoaji misaada nchini Nigeria zimetangaza kuwa, kuna uwezekano wa kuongezeka wahanga wa ajali hiyo kutokana na hali za baadhi ya majeruhi wa mlipuko huo kuwa mbaya. Mmoja wa maafisa wa jimbo hilo ameziambia duru za habari kwamba, ni miili mitatu tu imeweza kutambuliwa kwani 14 iliyobakia imeungua kabisa.

Miripuko ya malori na mabomba ya kusafirishia mafuta na gesi imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, taifa la Afrika magharibi lenye utajiri wa bidhaa hizo.

Mwaka 2020 makumi ya watu walipoteza maisha katika mripuko wa lori la mafuta katika eneo la Odukpani, jimboni Cross River kusini mashariki mwa Nigeria.

Mwaka 2019 zaidi ya watu 60 waliokuwa wakijaribu kuchota mafuta baada ya lori la mafuta kuripuka waliaga dunia katika mkasa huo.

Kadhalika Machi mwaka jana, mripuko wa bomba la gesi uliotokea katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos nchini Nigeria ulipelekea watu 15 kuaga dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Aidha Juni mwaka 2015 karibu watu 70 walifariki huko mashariki mwa Nigeria mjini Onitsha baada ya lori la kubeba mafuta kushika moto.

342/